갈라디아서 3장 Swahili NT
- 1 Enyi Wagalatia, mmekuwa wajinga kweli! Ni nani aliyewaloga? Habari juu ya kusulubiwa kwake Yesu Kristo ilielezwa waziwazi mbele ya macho yenu.
- 2 Napenda kujua tu kitu kimoja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa sababu ya kutimiza matakwa ya Sheria ama kwa sababu ya kuisikia na kuiamini Habari Njema?
- 3 Je, mu wajinga kiasi hicho? Ninyi mlianza yote kwa msaada wa Roho je, mnataka sasa kumaliza kwa nguvu zenu wenyewe?
- 4 Je, mambo yale yote yaliyowapata ninyi yamekuwa bure tu? Haiwezekani!
- 5 Je, Mungu huwajalia Roho na kutenda miujiza kati yenu ati kwa sababu mnatimiza yanayotakiwa na sheria, ama kwa sababu mnasikia Habari Njema na kuiamini?
- 6 Chukueni kwa mfano habari za Abrahamu: yeye alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.
- 7 Sasa basi jueni kwamba watu wenye kumwamini ndio walio watoto halisi wa Abrahamu.
- 8 Maandiko Matakatifu yalionyesha kabla kwamba Mungu atawakubali watu wa mataifa kuwa waadilifu kwa njia ya imani. Hivyo Maandiko Matakatifu yalitangulia kumtangazia Abrahamu Habari Njema: "Katika wewe mataifa yote yatabarikiwa."
- 9 Basi, wale walio na imani wanabarikiwa pamoja na Abrahamu aliyeamini.
- 10 Lakini wote wanaotegemea tu kutimiza yanayotakiwa na Sheria, wako chini ya laana. Maana, Maandiko Matakatifu yasema: "Yeyote asiyeshika na kutimiza yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Sheria, yuko chini ya laana."
- 11 Ni dhahiri kwamba Sheria haiwezi kumfanya mtu akubaliwe kuwa mwadilifu; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Mwadilifu kwa imani ataishi."
- 12 Lakini Sheria haitegemei imani, ila Maandiko yasema: "Mwenye kutimiza yanayotakiwa na Sheria ataishi."
- 13 Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya Sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: "Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa."
- 14 Jambo hili lilifanyika kusudi ile baraka aliyopewa Abrahamu iwashukie watu wa mataifa mengine kwa njia ya Kristo, na ili kwa imani, tumpokee yule Roho ambaye Mungu alituahidia.
- 15 Ndugu, nitawapeni mfano kutoka maisha yetu ya kila siku. Fikirini juu ya mkataba kati ya watu wawili. Mkataba ukisha fanyika na kutiwa sahihi hapana mtu anayeuweka kando au kuuongezea kitu.
- 16 Basi, Abrahamu alipewa ahadi, yeye pamoja na mzawa wake. Maandiko hayasemi: "Na wazawa wake," yaani wengi, bali yasema, "Na mzawa wake," yaani mmoja, naye ndiye Kristo.
- 17 Ninachotaka kusema ni hiki: Mungu alifanya agano lake akalithibitisha; Sheria ambayo ilitokea miaka mia nne na thelathini baadaye, haiwezi kulitangua hilo agano wala kuibatilisha hiyo ahadi.
- 18 Maana, kama urithi ya Mungu inategemea Sheria, basi, haiwezi kutegemea tena ahadi ya Mungu. Kumbe, lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa sababu aliahidi.
- 19 Ya nini basi, Sheria? Iliongezwa hapo ili kuonyesha uhalifu ni kitu gani, mpaka atakapokuja yule mzawa wa Abrahamu aliyepewa ile ahadi. Sheria ililetwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi.
- 20 Ama hakika, mpatanishi hahitajiwi ikiwa jambo lenyewe lamhusu mtu mmoja; na Mungu ni mmoja.
- 21 Je, Sheria inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria ambayo ingeweza kuwapa watu uzima, basi, tungeweza kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Sheria.
- 22 Lakini sivyo; Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala wa dhambi; na hivyo, kwa kumwamini Yesu Kristo, wenye kuamini watimiziwe ile ahadi.
- 23 Kabla ya kujaliwa imani, Sheria ilitufanya wafungwa mpaka imani hiyo iliyokuwa inakuja ifunuliwe.
- 24 Basi, hiyo Sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya imani, tukubaliwe kuwa waadilifu.
- 25 Tangu kufika kwa hiyo imani, Sheria si mlezi wetu tena.
- 26 Kwa njia ya imani, ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika kuungana na Kristo.
- 27 Ninyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo.
- 28 Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja katika kuungana na Kristo Yesu.
- 29 Ikiwa ninyi ni wa Kristo, basi ni wazawa wa Abrahamu, na mtapokea yale aliyoahidi Mungu.