갈라디아서 6장 Swahili NT
- 1 Ndugu, kama mkimwona mtu fulani amekosea, basi, ninyi mnaoongozwa na Roho mwonyeni mtu huyo ajirekebishe; lakini fanyeni hivyo kwa upole, mkiwa na tahadhari msije nanyi wenyewe mkajaribiwa.
- 2 Saidianeni kubeba mizigo yenu na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo.
- 3 Mtu akijiona kuwa ni kitu, na kumbe si kitu, huyo anajidanganya mwenyewe.
- 4 Lakini kila mmoja na aupime vizuri mwenendo wake mwenyewe. Ukiwa mwema, basi, anaweza kuona fahari juu ya alichofanya bila kuwa na sababu ya kujilinganisha na mtu mwingine.
- 5 Maana kila mmoja anao mzigo wake mwenyewe wa kubeba.
- 6 Mwenye kufundishwa neno la Mungu na amshirikishe mwalimu wake riziki zake.
- 7 Msidanganyike; Mungu hafanyiwi dhihaka. Alichopanda mtu ndicho atakachovuna.
- 8 Apandaye katika tamaa za kidunia, atavuna humo uharibifu; lakini akipanda katika Roho, atavuna kutoka kwa Roho uzima wa milele.
- 9 Basi, tusichoke kutenda mema; maana tusipolegea tutavuna mavuno kwa wakati wake.
- 10 Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema, na hasa ndugu wa imani yetu.
- 11 Tazameni jinsi nilivyoandika kwa herufi kubwa, kwa mkono wangu mwenyewe.
- 12 Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili ndio wanaotaka kuwalazimisha ninyi mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu moja tu: kusudi wao wenyewe wasije wakadhulumiwa kwa sababu ya msalaba wa Kristo.
- 13 Maana, hao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki Sheria; huwataka ninyi mtahiriwe wapate kujivunia alama hiyo mwilini mwenu.
- 14 Lakini mimi sitajivunia kamwe chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu.
- 15 Kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; cha maana ni kuwa kiumbe kipya.
- 16 Wanaoufuata mwongozo huo nawatakia amani na huruma; amani na huruma kwa Israeli--Wateule wa Mungu.
- 17 Basi, sasa mtu yeyote asinisumbue tena, maana alama nilizo nazo mwilini mwangu ni zile za Yesu.
- 18 Ndugu, nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Kristo. Amina.