에베소서 5장 Swahili NT
- 1 Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana ninyi ni watoto wake wapenzi.
- 2 Upendo uongoze maisha yenu, kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama dhabihu yenye harufu nzuri na tambiko impendezayo Mungu.
- 3 Kwa vile ninyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu.
- 4 Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa.
- 5 Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mfisadi, (ufisadi ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika Utawala wa Kristo na wa Mungu.
- 6 Msikubali kudanganywa na mtu kwa maneno matupu; maana, kwa sababu ya mambo kama hayo ghadhabu ya Mungu huwajia wote wasiomtii.
- 7 Basi, msishirikiane nao.
- 8 Zamani ninyi mlikuwa gizani, lakini sasa ninyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga:
- 9 maana matokeo ya mwanga ni wema kamili, uadilifu na ukweli.
- 10 Jaribuni kujua yale yanayompendeza Bwana.
- 11 Msishiriki katika matendo yasiyofaa, ya giza bali yafichueni.
- 12 Mambo yanayotendwa kwa siri ni aibu hata kuyataja.
- 13 Lakini mambo yale yanayotendwa katika mwanga, ukweli wake hudhihirishwa;
- 14 na kila kilichodhihirishwa huwa mwanga. Ndiyo maana Maandiko yasema: "Amka wewe uliyelala, fufuka kutoka wafu, naye Kristo atakuangaza."
- 15 Basi, muwe waangalifu jinsi mnavyoishi: Msiishi kama wapumbavu, bali kama wenye hekima.
- 16 Tumieni vizuri muda mlio nao maana siku hizi ni mbaya.
- 17 Kwa hiyo, msiwe wapumbavu, bali jaribuni kujua matakwa ya Bwana.
- 18 Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu.
- 19 Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu.
- 20 Mshukuruni Mungu Baba daima kwa ajili ya yote, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
- 21 Kila mmoja amstahi mwenzake kwa sababu ya kumcha Kristo.
- 22 Wake wawatii waume zao kama kumtii Bwana.
- 23 Maana mume anayo mamlaka juu ya mkewe, kama vile Kristo alivyo na mamlaka juu ya kanisa; naye Kristo mwenyewe hulikomboa kanisa, mwili wake.
- 24 Kama vile kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo, wake wawatii waume zao katika mambo yote.
- 25 Nanyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa, akajitoa mwenyewe sadaka kwa ajili yake.
- 26 Alifanya hivyo, ili kwa neno lake, aliweke wakfu kwa Mungu, baada ya kulifanya safi kwa kuliosha katika maji,
- 27 kusudi ajipatie kanisa lililo takatifu na safu kabisa, kanisa lisilo na doa, kasoro au chochote cha namna hiyo.
- 28 Basi, waume wanapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe.
- 29 (Hakuna mtu yeyote auchukiaye mwili wake; badala ya kuuchukia, huulisha na kuuvika. Ndivyo naye Kristo anavyolitunza kanisa,
- 30 maana sisi ni viungo vya mwili wake.)
- 31 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Kwa hiyo, mwanamume atawaacha baba na mama yake, ataungana na mkewe, nao wawili watakuwa mwili mmoja."
- 32 Kuna ukweli uliofichika katika maneno haya, nami naona kwamba yamhusu Kristo na kanisa lake.
- 33 Lakini yanawahusu ninyi pia: kila mume lazima ampende mkewe kama nafsi yake mwenyewe, naye mke anapaswa kumstahi mumewe.