데살로니가후서 1장 Swahili NT
- 1 Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba yetu na wa Bwana Yesu Kristo.
- 2 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
- 3 Ndugu, tunapaswa kushukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Inafaa kwetu kufanya hivyo kwani imani yenu inakua sana na kupendana kwenu kunaongezeka sana.
- 4 Ndio maana sisi tunajivunia ninyi katika makanisa ya Mungu. Tunaona fahari juu ya jinsi mnavyoendelea kuamini na kustahimili katika udhalimu wote na mateso mnayopata.
- 5 Hayo yote yanathibitisha kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na matokeo yake ninyi mtastahili Utawala wake ambao kwa ajili yake mnateseka.
- 6 Mungu atafanya jambo la haki: atawalipa mateso wale wanaowatesa ninyi,
- 7 na kuwapeni nafuu ninyi mnaoteseka, na sisi pia. Atafanya jambo hilo wakati Bwana atakapotokea kutoka mbinguni pamoja na malaika wake na wakuu
- 8 na miali ya moto, kuwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu.
- 9 Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu,
- 10 wakati atakapokuja Siku ile kupokea utukufu kutoka kwa watu wake na heshima kutoka kwa wote wanaoamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwao, kwani mmeuamini ule ujumbe tuliowaletea.
- 11 Ndiyo maana tunawaombeeni daima. Tunamwomba Mungu wetu awawezeshe muyastahili maisha aliyowaitia myaishi. Tunamwomba, kwa uwezo wake, atimize nia yenu ya kutenda mema na kukamilisha kazi yenu ya imani.
- 12 Kwa namna hiyo, jina la Bwana wetu Yesu litapata utukufu kutoka kwenu, nanyi mtapata utukufu kutoka kwake kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.